Balozi alizungumza moja kwa moja na watoto, akiwapa maneno ya faraja, matumaini na motisha, akisisitiza kuwa maisha bora yanawezekana kwa bidii, nidhamu na msaada wa jamii.
Shirika la Habari la Kimataifa la Ahlul-Bayt (as) -ABNA- Tanga, Tanzania - Katika kuendeleza ushirikiano wa kirafiki kati ya Jamhuri ya Kisoshalisti ya Vietnam na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Balozi wa Vietnam nchini Tanzania alifanya ziara ya pekee katika Kituo cha Watoto Yatima cha "Goodwill and Humanity Foundation", kilichopo jijini Tanga, mnamo tarehe 24 Julai 2025.
Katika ziara hiyo yenye kugusa moyo, Balozi huyo alipokelewa kwa heshima kubwa na uongozi wa kituo pamoja na watoto yatima waliopo chini ya uangalizi wa taasisi hiyo. Akiwa amefuatana na baadhi ya maafisa wa ubalozi, Balozi alizunguka maeneo mbalimbali ya kituo hicho na kujionea hali halisi ya maisha ya watoto hao.
Maneno ya Faraja na Matumaini
Balozi alizungumza moja kwa moja na watoto, akiwapa maneno ya faraja, matumaini na motisha, akisisitiza kuwa maisha bora yanawezekana kwa bidii, nidhamu na msaada wa jamii. Alisema:
“Watoto hawa ni tunu ya jamii na ni jukumu letu sote kuhakikisha wanapata malezi bora, elimu nzuri na mazingira salama ya kukua. Vietnam iko tayari kushirikiana na taasisi kama hii kusaidia juhudi zenu.”
Misaada na Zawadi
Katika kuonesha mshikamano wa kidiplomasia na wa kibinadamu, Balozi alikabidhi misaada mbalimbali kwa kituo hicho ikiwemo:
1_ Vifaa vya shule (madaftari, kalamu, vitabu).
2_ Mavazi na viatu.
3_Vyakula vya msaada.
4_ Na michezo ya watoto.
Kauli za Uongozi wa Kituo
Mkurugenzi wa Goodwill and Humanity Foundation, Sayyid Muhdhari, alitoa shukrani zake kwa niaba ya taasisi, akisema:
“Ziara hii imetupa moyo mkubwa. Ni nadra sana kuona viongozi wa ngazi ya ubalozi wakijumuika na watoto wetu kwa upendo huu wa kweli. Tunathamini sana mshikamano huu wa kimataifa.”
Ushirikiano wa Baadaye
Balozi aliahidi kuwa ubalozi wa Vietnam utaendelea kuangalia uwezekano wa kusaidia kwa njia endelevu, ikiwemo usaidizi wa miradi ya elimu, afya na lishe kwa watoto yatima nchini Tanzania, hasa kupitia ushirikiano na taasisi za kijamii kama Goodwill Foundation.
Tukio hili limeacha alama kubwa ya matumaini, huruma na mshikamano wa kimataifa, likiwa ni mfano wa diplomasia ya huruma yenye tija kwa jamii za walio na uhitaji.
Your Comment